TANGAZO


Friday, March 27, 2015

Huku maandalizi ya Tamasha la Pasaka yakiwa yamekamilika kwa asilimia kubwa

*Malope, Mahlangu kutua Dar Aprili 4
Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama akifafanua jambo kwa waandishi wa habari jana, wakati alipokuwa akielezea kuhusu kukamilika kwa maandalizi ya Tamasha la Pasaka, litakalozinduliwa Aprili 5, mwaka huu, Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam. Kulia ni Mjumbe wa Kamati ya Maandalizi ya tamasha hilo, Jimmy Charles. (Picha na Kassim Mbarouk-www.bayana.blogspot.com)

Mwandishi Wetu
WAIMBAJI  wa kimataifa wa nyimbo za Injili, Rebecca Malope na Solly Mahlangu wanatarajiwa kuwasili Dar es Salaam Aprili 4, mwaka huu wakitokea Afrika Kusini tayari kwa kutumbuiza katika maadhimisho ya miaka 15 ya Tamasha la Pasaka.

Kwa mujibu wa taarifa ya Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya maandalizi ya tamasha hilo, maandalizi yamekamilika kwa kiasi kikubwa na kuwataka mashabiki wa muziki wa Injili kujitokeza kwa wingi kuwapa hamasa waimbaji watakaokuwepo na kupata ujumbe wa neno la Mungu.

Msama alisema mwimbaji mwingine raia wa Afrika Kusini, Solly Mahulangu naye pia anatarajia kuwasili Jumamosi akitokea Afrika Kusini na kundi lake ambalo litatoa burudani kwa wakazi wa Dar es Salaam.
"Tamasha la mwaka huu lina mambo mengi ambayo yataendana na miaka 15 ya tamasha hilo kubwa hapa Tanzania kwa sababu linashirikisha waimbaji wa Kimataifa na viongozi wakubwa serikalini ambao hufikisha ujumbe wa serikali na neno la Mungu pia," alisema Msama.

Msama alisema mwimbaji Mtanzania anyeishi Kenya, Faustine Munishi anatarajia kuwasili Aprili 3 kwa lengo la kufikisha ujumbe wa Neno la Mungu  kupitia waimbaji na viongozi wa dini watakaojitokeza uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.

Tamasha hilo litazinduliwa Aprili 5 mwaka huu, kwenye Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment