TANGAZO


Saturday, October 11, 2014

NHIF Yawapongeza viongozi wa Dini kwa kuhamasisha kaya kujiunga na CHF

Meneja Mwandamizi wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Kanda ya Magharibi – Tabora Bw. Emmanuel Adina akifafanua jambo kwa mwandishi wa habari (hayupo pichani) alipofanya mahojiahano maye wakati wa Maonyesho ya Wiki ya Vijana inayofanyika Kitaifa Mkoani Tabora.
Ofisa Masoko na Elimu kwa Umma wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Bibi Catherine Kameka akielezea jambo kuhusu Mfuko wa Afya ya Jamii (CHF) kwa wananchi walitembelea banda lao wakati wa Maonyesho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika Kitaifa Mkoani Tabora. 
Meneja Mwandamizi wa Mfuko wa Bima ya Afya (NHIF) Kanda ya Magharibi – Tabora Bw. Emmanuel Adina (kushoto) akifafanua jambo kwa Afisa Habari wa kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo Bw. Jonas Kamaleki alipofanya mahojiahano naye kuhusu Mfuko wa Afya ya Jamii unavyo nufaisha Vijana wakati wa Maonyesho ya Wiki ya Vijana inayofanyika Kitaifa Mkoani Tabora.
Baadhi ya wananchi wakipata huduma ya upimaji wa Afya inayotolewa bure na Mfuko wa Taifa waBima ya Afya (NHIF) katika Maonyesho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mjini Tabora.
Baadhi ya wananchi wakipata huduma ya upimaji wa Afya inayotolewa bure na Mfuko wa Taifa waBima ya Afya (NHIF) katika Maonyesho ya Wiki ya Vijana yanayoendelea mjini Tabora. (Picha zote na Frank Shija, Tabora)

Na Jonas Kamaleki, Tabora
VIONGOZI wa dini mkoani Tabora wametoa mchango mkubwa katika kuhamasisha waumini wao kujiunga na Mfuko wa Afya wa Jamii (CHF) na kuufanya mkoa huo kuwa katika hali nzuri ya watu wake kupata matibabu.

Hayo yamebainishwa na Meneja Mwandamizi wa Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) Kanda ya Magharibi-Tabora, Bw. Emmanuel Adina katika Maonyesho ya Wiki ya Vijana yanayofanyika Kitaifa mjini Tabora. 

Adina ameongeza kuwa viongozi wa dini zote wamekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha waumini wao kujiunga na CHF ili kuwa nauhakika wa kupata huduma stahiki ya matibabu.

Aidha amesema kuwa viongozi hao wamekuwa wakihamasisha watu wao misikitini, kwa upande wa Waislam na makanisani kwa Wakristo. 
Hadi sasa jumla ya kaya 38,000 wamejiunga na Mfuko huo huku lengo likiwa ni kufikia  asilimia 30 ya waliojiunga na CHF ifikapo Juni 2015,
Meneja huyo ameitaja wilaya ya Igunga kuongoza katika uhamasishaji wa wananchi kujiunga na CHF. “Namshukuru sanaMkuu wa Wilaya ya Igunga, Bw. Elibariki Kingu kwa mchango mkubwa anaoutoa kwa wana Igunga kujinga na Mfuko huo ambapo jumla ya kaya 9,000 wilayani Igunga zimejiunga na CHF ambayo ni idadi kubwa kutokana na uhamasishaji wa Mkuu wa wilaya”. Alisema Bw. Adina.

Ameongeza kuwa Bw. Adina amezitaja wilaya nyingine ambazo kaya nyingi zimejiunga na Mfuko huo kuwa ni Nzega, Uyui,Urambo na Sikonge. Katika wilaya hizo kinachosaidia zaidi watu kujiunga ni kuwepo wilayani humo vyama vya ushirika vya msingi vya tumbaku.

Zipo pia changamoto NHIF inayokutana nazo kuhusiana na wana Tabora kujiunga na CHF. Changamoto hizo Meneja huyo amezitaja kuwa ni kipato kidogo cha wakazi wa Tabora inayotokana kuwa baadhi ya wilaya hazina zao kuu la biashara la kuwapatia kipato cha uhakika, kutokuwepo na elimu ya kutosha ya mifumo ya Bima na pia ukosefu wa dawa na vifaa tiba katika mahospitali, zahanati na vituo vya afya.

Kwa upande mwingine, Afisa Masoko na Elimu kwa Umma wa NHIF, Bi Catherine Kameka amewataka wananchi wajiunge kwa wingi na Mfuko wa Afya wa Jamii na Bima ya Afya ili waepuke usumbufu wa kukosa matibabu wakati wanapokuwa wanahitaji matibabu na hawana pesa. Amesema ugonjwa hauna msimu, unaweza kujitokeza wakati wowote hivyo ukiwa kwenye mifumo ya Bima ni rahisi kuhudumiwa.


Ameongeza kuwa huduma zinazotolewa kwa wanachama wa NHIF zimeboreshwa na kuvutia wanachama wengi zaidi ikilinganishwa na ilivyokuwa wakati mfuko unaanzishwa. Hivyo amewataka wanaTabora wachangamkie fursa hiyo ili wawe na afya njema wakati wote kwa maana mtu akiwa na afya safi anaweza kujishughulisha kikamilifu katika shughuli za uzalishaji mali.

No comments:

Post a Comment