Ofisa Habari na Mawasiliano, Munir Shemweta toka Tume ya Kurekebisha
Sheria Tanzania, akizungumza na waandishi wa habari juu
ya faida za kuimarishwa kwa mfumo wa sheria wa huduma za jamii kwa wazee
utakaowezesha upatikanaji wa huduma muhimu za maisha kwa kundi hilo, Jijini Dar es Salaam. Katikati ni Ofisa Habari
toka Idara ya Habari, Frank Mvungi na kulia ni Ofisa Sheria Mkuu wa Tume
hiyo, Anjela Shila.
Ofisa Sheria Mkuu toka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Anjela Shila (kulia), akisisitiza jambo juu ya faida za kuimarishwa kwa mfumo wa sheria wa huduma za jamii kwa wazee utakaowezesha upatikanaji wa huduma muhimu za maisha kwa kundi hilo, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam.
Katibu Msaidizi Elimu ya Sheria kwa Umma toka Tume ya
Kurekebisha Sheria Tanzania, Agnes Mgeyekwa (kushoto), akitoa ufafafanuzi
kuhusu namna tume hiyo, inavyotimiza majukumu yake katika kurekebisha sheria
mbalimbali nchini, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Ofisa Habari na Mawasiliano wa tume hiyo, Munir Shemweta.
Katibu Msaidizi Elimu ya Sheria kwa Umma toka Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania, Agnes Mgeyekwa (kushoto), akitoa ufafafanuzi kuhusu namna tume hiyo, inavyotimiza majukumu yake katika kurekebisha sheria mbalimbali nchini, wakati wa mkutano na waandishi wa habari Jijini Dar es Salaam leo. Kulia ni Ofisa Habari na Mawasiliano wa tume hiyo, Munir Shemweta.
Tume ya
Kurekebisha Sheria Tanzania imeanza kupitia mfumo wa sheria wa huduma za jamii
kwa wazee (elderly social care) kwa nia ya kubaini mapungufu yaliyoko kwenye
mfumo huo na kutoa mapendekezo stahiki
ili kuweza kuwa na mfumo mzuri wa sheria
utakaolenga ustawi na hifadhi kwa wazee wote waliohitimu miaka 60 na
zaidi wa mijini na vijijini.
Wazee
wanapofikia umri mkubwa, uwezo wao wa kujihusisha na shughuli mbalimbali
hupungua na hivyo hushindwa kijihudumia mahitaji yao muhimu ya kila siku kama
vile chakula, mavazi, malazi, pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali za
ujenzi wa taifa ziwe za kitamaduni, kijamii au kiuchumi.
Tume imeona
kuna umuhimu wa kuimarisha mfumo wa sheria
wa huduma za jamii kwa wazee ili kuwezesha wao kupata huduma muhimu za maisha. Pamoja na kuwa na Sera ya Taifa ya Wazee
(National Ageing Policy, 2003) Tanzania haina sheria maalum katika eneo
hili. Sheria mbalimbali za mafao
zinawagusa wazee wanaostaafu kazi serikalini na sekta binafsi ambao ni sehemu
ndogo sana ya kundi la wazee wengi wanaokosa huduma muhimu za maisha.
Ikumbukwe kuwa wazee hawa ni wale waliotumikia taifa kwa
nguvu na moyo wote kwenye ngazi mbalimbali wakati wakiwa na nguvu zao hivyo
wanapokuwa wamezeeka ni muhimu wakawekewa mfumo bora wa kisheria ili kuhakikisha
wanaishi maisha mazuri bila kujali kupungua kwa uwezo wao wa kujishughulisha
katika nyanja mbalimbali.
Kwa sasa Tume inaendelea na rasimu ya awali ya kuangalia
hali halisi ya Tanzania kuhusiana na suala zima la wazee ikiwemo mikataba ya
kimataifa, mifumo ya kisheria na kijamii pamoja na sera na na baada ya hapo
itatembelea mikoa mbalimbali ya Tanzania bara kwa nia ya kukusanya maoni ya
wananchi juu ya mfumo huo wa kisheria.
Maoni hayo yatahusisha wazee wenyewe, maofisa kazi, afya, ustawi wa
jamii, watendaji wa vijiji, taasisi zisizokuwa za kiserikali
zinazojishughulisha na wazee pamoja na wananchi kwa ujumla.
Ni Matarajio ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania kuwa
baada ya kukamilika kwa mapitio ya mfumo huo wa kisheria kuhusiana na huduma za
jamii kwa wazee, Tume itakuja na mapendekezo ya kisheria na yasiyo ya kisheria
ambayo yataleta tija kwa taifa kwa ujumla.
Kuhusu
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania
Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania ni Idara ya Serikali
inayojitegemea chini ya Wizara ya Katiba na Sheria. Ilianzishwa kwa mujibu wa sheria kupitia
kifungu cha 3 cha Sheria ya Tume ya Kurekebisha Sheria, Namba 11 ya mwaka
1980. Sheria hii kwa sasa ni Sura ya 171
ya Sheria za Tanzania kama sheria zilivyorekebishwa katika toleo la mwaka
2002.
Majukumu ya Tume katika ujumla wake ni kutoa mapendekezo
ya marekebisho ya Sheria mbalimbali kwa Serikali, kwa kutafiti na kutathmini
maeneo yote ya sheria husika na kuyatolea mapendekezo kwa lengo la
kuyaboresha. Baada ya utafiti, Tume
huwasilisha taarifa yake kwa Waziri anayehusika na masuala ya sheria.
Moja ya mafanikio ya Tume yaliyopatikana kutokana na mapendekezo ya Taarifa
zake zinazopelekwa kwa Waziri anayehusika na masuala ya sheria ni pamoja na
kutungwa kwa sheria mbalimbali ikiwa ni pamoja na:-
·
Marekebisho ya
Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 1985 Kuhusu Kuwalipa Fidia
Wahanga Wa Makosa Ya Jinai;
·
Kuchapishwa kwa
Tangazo la Serikali Na. 192 la mwaka 1988 kuhusu Uharakishwaji wa Mashauri
Mahakamani;
·
Mapitio ya Sheria
ya Udhibiti wa Ubadilishaji wa Fedha za Kigeni;
·
Uanzishwaji wa
Mfumo wa Wafungwa Kutumikia Sehemu ya Vifungo Nje ya Gereza;
·
Marekebisho Makubwa
Yalifanywa Kwenye Sheria 28 Kati ya 40 Zilizopendekezwa na Tume ya Nyalali
Ikiwa ni Sehemu ya Mapendekezo Yaliyotolewa na Tume ya Kurekebisha Sheria Baada
ya Kusoma Taarifa Hiyo ya Tume ya Nyalali
·
Kutungwa kwa Sheria
ya “Makosa ya Kujamiiana” Na. 4 ya 1998;’
·
Marekebisho ya
Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Madai Ili Kutambua Utatuzi wa Migogoro kwa
Njia za Usuluhishi;
·
Kutungwa kwa Sheria
za Kazi za Mwaka 2004;
·
Kurekebishwa Sheria
ya Ushahidi Ili Kutambua Ushahidi wa TEKNOHAMA (Electronic Evidence) Mwaka 2007;
·
Kutungwa kwa Sheria
ya Vinasaba vya BinadamuMwaka 2009;
·
Kutungwa kwa Kanuni
Mpya za Mahakama ya Rufaa (Court of Appeal Rules) za Mwaka 2009
·
Kutungwa kwa Sheria
Zinazohusu Haki za Watu Wenye Ulemavu za Mwaka 2009;na
·
Kutungwa kwa Sheria
ya Mtoto ya Mwaka 2009.
Imetolewa
na:
Munir Shemweta
Afisa Habari na Mawasiliano
TUME
YA KUREKEBISHA SHERIA TANZANIA
27
JULAI 2013
No comments:
Post a Comment